TBA na dhamira ya kuibadili Dodoma kuwa kama Ulaya

Sdílet
Vložit
  • čas přidán 28. 01. 2024
  • Mwaka 2016 aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alitangaza uamuzi wa Serikali yake kutoka Dar es Salaam kuhamishia ofisi zake jijini Dodoma ikiwemo Ikulu.
    Maamuzi hayo yalitajwa kama kutekeleza azma ya waasisi wa taifa hili waliotaka Serikali iishi huko ambapo kimsingi ndio katikati ya nchi.
    Baada ya uamuzi huo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliipatia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), dhamana ya ubunifu na usanifu katika mji wa Serikali Mtumba.
    TBA ilipewa kazi ya kubuni kwa awamu mbili ikiwa ni ubunifu wa majengo ya chini kuharakisha shughuli za Serikali kuanza. Mwaka 2019 hadi 2020 majengo yalikamilika na yalizinduliwa na Hayati Magufuli.
    Awamu ya pili ilikuwa ni usanifu wa ujenzi wa majengo ya Serikali yenye kubeba watumishi wote ambapo ujenzi ulianza mwaka 2021.
    Akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, Mkurugenzi wa Ujenzi TBA, Mhandisi Wenceslaus Kizaba, anasema awali walizingatia mipango miji ya mji wa Serikali, muongozo wa ofisi ya Rais pamoja na mahitaji ya wizara na taasisi zake.
    Mbali na hiyo anasema TBA katika ubunifu walizingatia pia mifumo ya Tehama, sambamba na taarifa ya uchunguzi wa udongo katika eneo la Mtumba.
    Mhandisi anasema kwakuwa Dodoma ipo kwenye ukanda wa matetemeko ya ardhi walizingatia kwanza uchunguzi kuhusu hali hiyo.
    Anasema walishirikiana na Tanroads, Taasisi ya Jiolojia, pamoja na Idara ya Jiolojia chuo kikuu cha Dar es Salaam kufanya upembuzi yakinifu kuja na taarifa ya matetemeko na kutoa muongozo wa majengo.
    Anasema uchunguzi ulitaka majengo msingi uanzie mita 3.5 kwenda chini na urefu usiwe chini ya ghorofa sita kwenda hadi 10.
    Hiyo inatokana na jengo likiwa fupi linaathirika sana wakati wa tetemeko lakini likiwa refu linahimiri hali hiyo.
    Mbali na matetemeko anasema walizingatia pia mfumo wa kukabiliana na majanga ya moto. Wamezingatia maelekezo ya idara ya zima moto ikiwemo uwepo wa ‘fire hydrants’.
    Mhandisi Kizaba anasema wameubuni mji kwa kuzingatia uvunaji wa maji ya mvua pamoja na umeme jua ambapo maji yatatumika kumwagilia bustani na endapo moto utatokea.
    Anasema wamefanya hivyo ili kuipunguzia Serikali gharama katika kuendesha majengo yake.
    Mhandisi anasema hadi sasa majengo mengi yaliyoanza Septemba 2021 yamefikia asilimia 75 hadi 97. Pia yaliyoanza Desemba 2021 yamefikia asilimia 60 hadi 75. Na yale yaliyoanza Januari 2023 yamefikia 35 hadi 40.
    Anasema vilevile kuna viwanja vya michezo, hoteli, maeneo ya biashara ambapo zitajengwa baada ya mwaka 2025 kukamilika kwa awamu ya kwanza.
    Anasema mbali na majengo kukamilika lakini pia utajengwa mnara mkubwa ambao mtu akipanda ataiona Dodoma nzima.

Komentáře •